Na Hawa Mohamed
na Tulinkisa Ndelwa
Kijiji cha
Luganga katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Vijijini kina wakulima wengi wa
pilipili, Wakulima hao wanakabiliwa na changamoto kadhaa katika kuwa na soko la
uhakika la zao la pilipili mbuzi.
Changamoto moja
inatokana na ulimbukeni wa kukurupuka kulima pilipili kwa wingi kwa kutarajia
kuwa bei nzuri ya msimu uliopita ndiyo itakuwa bei ya msimu unaofuata. Wakulima
hao wamejikuta wakiingia katika mkumbo wa kuchangamkia kilimo cha pilipili
mbuzi kutokana na msimu mzuri uliopita.Wakulima wengi hubabaika na hulima
wakiangalia zao lenye bei nzuri na pindi bei inapoporomoka na kuwatia hasara
wakulima hao huamua kuachana na pilipili mbuzi kabisa.
Mbali na hasara
inayoweza kumkuta mkulima kwa kulima kwa wingi kwa matarajio ya bei kubwa na
hivyo kuchangia mavuno kufurika na kuharibu bei, wakulima pia hukabiliwa na
kutofahamu yaliko masoko ya bidhaa yao na hivyo kulazimika kutegemea
wafanyabiashara wa kati – madalali. Madalali hao hununua pilipili mbuzi kwa bei
ndogo kutoka kwa wakulima na kisha kuiuza kwa wafanyabiashara wengine kwa bei
kubwa.
Mkulima YOHANES JUMANNE katika kijiji cha luganga,
aliongea na IBER akasema alijiikuta anashindwa kung'ang'ania bei ambayo ni
kinyume na matakwa ya madalili. Aisema moja ya vitu vinavyomfanya akose nguvu
ya kudai bei bora zaidi ni kwamba soko linakuwa limefurika kiasi cha kuwafanya
wakulima wengine kuachana kabisa na kilimo cha pilipili mbuzi. Aliongezea na
kusema ufumbuzi unaweza kuwa eneo ambalo linatambulika wazi kuwa ni soko la
pilipili mbuzi.
Kuwepo kwa soko
la kudumu ni kitu ambacho kinaweza kumsaidia mkulima kupata kipato zaidi. Bei
ya mazao inakuwa ni yakueleweka kwa kuwa hakutakuwa na madalali, wakulima
watapata fursa ya kujiendesha wenyewe pia inaongeza ujuzi na maarifa juu ya
soko na biashara kutokana na uwepo wa wataalamu juu ya masoko.
FIKIRA KISSIMBA
ni Katibu Tawala Msaidizi, Uchumi na Uzalishaji, mkoa wa Iringa. Yeye alisema
wakulima wasioweza kupata wateja wa mazao yao kwa haraka wanapaswa kuwa na eneo
ambako ndio pekee pauziwe mazao yao.
Mindombinu ya
uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi na usindikaji ni muhimu katika kuimarisha
uhakika wa masoko ya mazao ya kilimo. Japo bado kuna changamoto ya uelewa mdogo
kwa wakulima. Licha ya kuwepo vikundi mbalimbali vya wakulima, bado ni wakulima
hawajajiunga kwenye vikundi hivyo huathiri utendaji wa wataalamu wa kilimo.
Jambo hili pia huchangia kukosekana kwa taarifa muhimu ikiwemo namna ya
kukabiliana na changamoto zinazowakumba wakulima. Lakini wakulima wanapojiunga katika
vikundi huku kila mmoja akiwa na mawazo tofauti na mwenzake, hupelekea
kushindwa kuafikiana. Kumbe, kama anavyoeleza Katibu Tawala Fikira Kissimba,
vikundi vyenye maafikiano vinaweza kusaidiwa mbinu mbalimbali zinaoweza
kukabiliana na kufurika kwa soko, ikiwa ni pamoja na usindikaji wa mavuno ya
ziada.
Faida ya
wakulima kuwa kwenye vikundi inakwenda mbali zaidi kuliko kuwapa nguvu kwenye
soko. Kuwa pamoja kunaisaidia serikali au wadau wengine kuwafikia wakulima kwa
urahisi ili kutoa usaidizi wa kitaalamu wa kuboresha zao lao.
Nae Afisa
Kilimo kata ya Ilolo Mpya, BWANA PETER SHAYO, alisema serikali inaweza kuwa na
usaidizi mzuri kwa wakulima iwapo watalima pamoja katika vikundi. Anasema hilo
linaweza kusaidia hata kwenye upatikanaji wa madawa.
Matokeo ya
piilipili kufurika katika soko hupelekea kuingia kwa madalali ambao
wanawanyonya wakulima kwa kuwabana kwenye bei ya shambani.
Nini kifanyike?
Kutengwa
maeneo mahususi kwa uuzaji na ununuaji wa pilipili kutawapa wakulima
uhakika wa soko na kujikinga na madalali wanaowanyonya. Nguvu ya wakulima pia
inaongezeka kwa kuwa kwenye vikundi na hivyo kutohitaji madalali, kwa kuwa pia
wanaweza kusaidiwa mikopo, madawa na ushauri na wadau wasiowanyonya. Na pia
wakulima kupatiwa ustadi wa kusindika mavuno ya ziada.
Mzigo wa
kuboresha soko kwa zao lao hilo, kwa sehemu kubwa limo mikononi mwa wakulima
wenyewe. Wawe na ushirikiano ili wawe na nguvu na pia waweze kupata usaidizi.
No comments:
Post a Comment