UVUVI HARAMU UNAVYOTOKOMEZA SAMAKI BWAWA LA MTERA-IRINGA
wavuvi katika bwawa la Mtera
Na Hawa Mohamed na Tulinkisa Ndelwa
Uvuvi ni mojawapo ya shughuli za binadamu ambayo ina shughulika na ukamataji wa samaki kutoka ndani ya maji na kuwekwa nje ya maji na samaki hutumika kama kitoweo na pia biashara ili kujipatia kipato nakukuza uchumi wa nchi.
Katika miaka ya hivi karibuni kumekua na ongezeko kubwa la uvuvi haramu katika maeneo mengi nchini likiwemo bwawa la Mtera lililopo mkoani Iringa na katika mkoa wa Dodoma.Uvuvi huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuadimika kwa samaki.
Sekta ya uvuvi ni moja ya sekta muhimu katika kuwapatia kipato Wananchi wengi wanaoishi kuzunguka bwawa la Mtera na hivyo kuwaondolea umaskini licha ya kuwa asilimia kubwa ya jamii hii ya wavuvi ni maskini jambo ambalo linapelekea wengi wao kujiingiza katika uvuvi haramu.
DABLA SINDOMBA na SAID MWAKIPESILE ni miongoni mwa wavuvi katika bwawa la mtera wao wanasema hali ngumu ya kiuchumi ndio hasa inayopelekea wengi wao kujiingiza katika uvuvi haramu kwa kutumia nyavu aina ya kokora.hawa ni wavuvi wadogo ambao wanategemea shughuli za uvuvi pekee katika kuendesha maisha yao.
Jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanywa na serikali ili kudhibiti uvuvi haramu katika bwawa la Mtera mkoani Iringa ikiwa ni pamoja na kufanya doria za mara kwa mara,Afisa uvuvi wa eneo la Migoli-Mtera ONESMO MINGA anasema licha ya doria wanazofanya kukamata wavuvi haramu, miti inayoota ndani ya bwawa hilo inasaidia kwa kuwakwamisha wavuvi kufanya uvuvi haramu katika baadhi ya maeneo ya bwawa hilo.
Katika Taarifa iliyotolewa na Afisa uvuvi mwandamizi BARACK CHIMBILA kutoka idara ya uvuvi Wilaya ya Iringa inaonesha kiasi cha samaki katika bwawa la Mtera mkoani Iringa kimepungua kutoka tani bil.96 laki sita na 35 elfu hadi tani mil.23 elfu laki saba na 82, katika kipindi cha mwaka 2014-2015 na hii ikichangiwa na uvuvi haramu uliokua ukiendeshwa katika bwawa la Mtera pamoja na kukauka kwa maji katika bwawa hilo.
Na kwa upande wake Afisa uvuvi mwandamizi mkoa wa Iringa PETER NYAKIGERA anasema jitihada za kutomeza uvuvi haramu katika bwawa la mtera zimekua hazileti matokeo mazuri kutokana na kuwa bwawa hilo limegawanyika katika mikoa miwili ambayo ni mkoa wa Iringa na mkoa wa Dodoma hivyo ni lazima kuwepo mikakati ya pamoja baina ya mikoa hiyo miwili.
Pamoja na jitihada ambazo zinafanywa na serikali na wadau mbalimbali katika kutokomeza uvuvi haramu bado vifaa vinavyotumika kufanya shughuli hizo zikiwemo nyavu aina ya kokora zimekua zikipatikana na kuuzwa kwa wavuvi jambo ambalo limekua likichochea kwa kiasi kikubwa uvuvi haramu. Vita dhidi ya uvuvi haramu iende sambamba na kudhibiti uingizaji wa zana zinazotumika katika shughuli za uvuvi haramu.
No comments:
Post a Comment